NDOA ni kuvumiliana na bila uvumilivu ndoa haiwezi kufaulu. Kuvumilia
kunamaanisha kukubali hali mbaya na ngumu ambazo hazifurahishi mtu.
Hasa, hali hizi huwa ni ngumu na nzito sana zinazoumiza mtu. Ni hali
ambazo mtu huwa hakuwa amezoea kabla ya kuingia katika ndoa au
kutarajia kupata katika ndoa. Baadhi ya shida huwa zinasababishwa na
mchumba wake au kuzuka kutokana na hali ambazo haziepukikikamwe.
Mtu pia anaweza kusababisha hali ngumu katika ndoa yake.
Ingawa wanandoa wanafaa kuvumiliana, kiwango cha uvumilivu na
mipaka yake pia kinapaswa kuzingatiwa ipasavyo.
Kuna shida zinazoweza kuvumiliwa kwa muda mrefu hadi hali ibadilike
na kuwa bora na kuna zile ambazo hata zikivumiliwa mtu hawezi kupata
afueni. Wakati mwingine watu huwa wanavumilia hali ambazo
zinawaweka kwenye hatari na kwa kufanya hivyo uvumilivu wao huwa
wa upofu.
Kuvumilia mume au mkeo akiwa mgonjwa au akipoteza kazi ni jambo
nzuri na la kupongezwa. Hii ndiyo aina ya uvumilivu wa kiapo cha ndoa.
Huu ni uvumilivu unaotokana na mapenzi ya dhati, pale mume na mke
wanasaidiana huku wakipitia hali ngumu ya uchumi na maradhi. Itakuwa
kukiuka kiapo cha ndoa iwapo sio ukatili mtu kuacha mumewe au
mkewe akiwa mgonjwa akisema amekuwa mzigo kwake. Lakini hii ni
tofauti na mtu kuvumilia mtu anayemtesa kimakusudi hima kimwili au
kisaikolojia. Kuna watu wanaovumilia kushambuliwa kimwili na
kisaikolojia na wachumba wao hadi wanaathirika kiafya na hata
kulemazwa. Kuvumilia mateso ya aina hii ni kilele kikubwa cha
upumbavu.
Kuna wanaume na wanawake wanaovumilia mateso kutoka kwa
wachumba wao hadi kaburini na kuwaacha waliowatesa wakiendelea na
maisha.
Katika kisa kimoja, mwanamke alivumilia madharau ya mumewe
kuwaleta wanawake tofauti kulala nao katika kitanda cha ndoa huku
akiamrishwa kulala kwenye kochi. Hatimaye mwanamume huyo
aliambukizwa Ukimwi na kufariki akiwa amepitisha kwa mkewe. Kama
mwanamke huyo hangevumilia kijinga na kujiondoa katika ndoa,
pengine hangejipata katika hali ya kuhuzunisha ya kuachwa mjane
anayeishi na Ukimwi.
Hata kama uvumilivu ni muhimu katika ndoa, unafaa kukitwa kwa busara
na hekima, haufai kuwa wa kienyeji tu eti kwa kuheshimu kiapo cha
ndoa. Itakuwa ujinga kuheshimu kiapo cha ndoa yako na mtu ambaye
hakiheshimu na hakuheshimu.
Vumilia ndoa yako na mtu anayekuheshimu lakini usivumilie katili
anayeweza kukupeleka kaburini na kuachwa akiendelea kufurahia
maisha yake kana kwamba haukuwahi kuwa katika maisha yake au
katika dunia hii.
Maisha ni yako na yake ni yake, kinachowaunganisha ni upendo na
kukutumbukiza katika mateso kunaonyesha upendo wake kwako
umetoweka.
Mambo ni mawili; waume wapende wake zao, wawajibike na kuheshimu
ndoa iwapo wanataka wawavumilie hali ngumu zinapozuka. Wake nao
waheshimu waume zao hata wakiwa wadhaifu na katika mazingira haya
ndoa zidumu na kuwa na furaha kwao wote
NA IKUMBUKWE SIKU ZOTE KWAMBA HESHIMA SIYO UTUMWA.