WAMILIKI wa biashara ndogo kama vile mama mboga na wahudumu wa bodaboda ni miongoni mwa Wakenya watakaofinywa na makali ya ushuru uliopendekezwa na bajeti ya kwanza ya Rais William Ruto.
Iwapo Mswada wa Fedha wa 2023 utapitishwa na Bunge, wamiliki wa biashara ndogo ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za angalau Sh1,400 kwa siku watalazimika kulipa asilimia tatu ya mauzo hayo.
Ikiwa mfanyabiashara anatoa huduma au bidhaa za Sh1,400 kila siku inamaanisha kwamba atatoa ushuru wa Sh15,000 kufikia Juni 31, 2024. Mfanyabiashara huyo atatozwa ushuru huo bila kujali ikiwa alipata faida au la.
Rais Ruto alipunguza kiasi cha mapato ya biashara yanayofaa kutozwa ushuru kwa mwaka kutoka Sh1 milioni hadi Sh500,000. Hiyo inamaanisha kuwa wafanyabiashara wadogo kama vile mama mboga, bodaboda au wamiliki wa vibanda watanaswa na ‘mtego’ huo.
Serikali pia imependekeza kuajiri maajenti watakaowinda mama-mboga, wachuuzi na wafanyabiashara wadogo wanaouza bidhaa zao kwenye vibanda kuhakikisha kuwa wanalipa ushuru.
Ripoti ya Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) inaonyesha kuwa serikali huenda ikajipatia ushuru wa hadi Sh2.8 trilioni endapo itanasa wafanyabiashara wadogo, wakiwemo jua-kali, mama-mboga, wahudumu wa bodaboda, wachuuzi kati ya wengineo.
Ushuru wa serikali ya Kenya Kwanza pia utaumiza zaidi Wakenya walalahoi ambao wamekuwa wakijipa mapato kwa kucheza kamari kama vile kutabiri matokeo ya mechi.
Ushuru kwa washindi wa kamari umeongezwa kutoka asilimia 7.5 hadi 20.
Hiyo ina maana kwamba ukitabiri matokeo ya mechi na kushinda Sh1,000, utapokea Sh800 na kiasi kilichosalia kitaelekezwa kwa serikali.
Baadhi ya bidhaa zilizokuwa zimeondolewa ushuru na serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambazo sasa zitaanza kutozwa ushuru wa asilimia 16 ni maziwa ya watoto na maeneo ya watu kupumzika.
Ushuru wa petroli, dizeli na mafuta taa umeongezwa kutoka asilimia 8 hadi 16 –hali ambayo itaongezea wananchi mzigo zaidi.
Kupanda kwa bei ya mafuta kutasababisha magari ya umma kuongeza nauli, ongezeko la bei ya umeme na bidhaa nyinginezo kama vile mkate na sukari. Wakenya ambao wamekuwa wakijikimu kupitia mikopo ya simu kutoka kwa kampuni kama vile Tala, Branch na nyinginezo nao hawajasazwa. Mikopo hiyo sasa itatozwa ushuru wa asilimia 20 kutoka asilimia 7.5.
Hata hivyo, haijulikani ikiwa ushuru wa mkopo wa Hustler Fund unaosimamiwa na serikali pia utatozwa asilimia 20 au la.
Japo ushuru wa huduma za simu na intaneti umepunguzwa kutoka asilimia 20 hadi 15, itakuwa ghali zaidi kutuma au kupokea hela kwa njia ya simu.
Ushuru wa huduma za kutuma hela kwa simu kama vile kutumia M-Pesa au Airtel Money, umeongezwa kutoka asilimia 12 hadi 15.
Ushuru mpya wa Rais Ruto pia utaumiza wafanyakazi walioajiriwa serikalini au mashirika ya kibinafsi.
Rais Ruto amependekeza ushuru huo kwa lengo la kukusanya Sh50 bilioni anazohitaji kujaza pengo la bajeti yake ya kwanza tangu kuchukua hatamu za uongozi.
Wakenya walioajiriwa watalazimika kukatwa asilimia 3 ya mishahara yao kufadhili mradi wa ujenzi wa nyumba nafuu. Waajiri nao wataongezea asilimia 3 juu ya kiasi hicho.
Wataalamu wameonya kuwa makato hayo ya nyumba nafuu huenda yakasababisha waajiri kupunguza idadi ya wafanyakazi au kukataa kuajiri.
Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) pia limepinga vikali makato hayo ya nyumba.
Chama cha watengenezaji wa bidhaa kinasema kuwa ushuru unaopendekezwa katika mswada huo, huenda ukasababisha kampuni, hasa katika sekta ya simiti, vyuma na karatasi kugura Kenya na kuhamia katika nchi jirani. Maafisa wa Chama cha Watengenezaji Bidhaa (KAM) walipofika mbele ya kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji, walisema kuwa mswada wa Fedha ukipitishwa, watu zaidi ya 100,000 katika sekta ya viwanda huenda wakafutwa kazi.
KENYA NCHI YETU SOTE.